NDUGAI AWAKARIBISHA MBOWE NA MATIKO ".....TUNASEMA WALIKUWA MTERA”
Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemkaribisha Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuendelea na shughuli za kibunge huku akisema kwa lugha ya kibunge walikuwa Mtera.
Mbali na Mbowe mwingine ni mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko ambao kwa pamoja walikuwa mahabusu katika gereza la Segerea baada ya kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, Machi 7, 2019 Mahakam Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliwarejeshea dhamana yao, baada ya kushinda rufaa waliyoikata wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu.
Baada ya kutoka, wawili hao leo Machi 12, 2019 wamekwenda bungeni kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango anawasilisha mapendekezo ya Serikali ya Mpango, Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Kabla Waziri Mpango hajaanza kuwasilisha taarifa yake katika ukumbi wa Pius Msekwa, Spika Ndugai alisema, "Kwanza nianze kwa kumkaribisha kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni (Mbowe) na mheshimiwa Esther Matiko kwa lugha ya kibunge tunasema walikuwa Mtera," amesema.
Hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kabla ya kuanza kuongea naye aliwakaribisha bungeni na kusema ni matumaini yake Mungu atasaidia wahudhuriwe kwa kadri inavyotakiwa.
Mbowe na Matiko hawakuhudhuria vikao vya mkutano wa 14.
Awali Mbowe na Matiko walionekana wakikumbatiana na wabunge mbalimbali wa CCM na upinzani.
Aidha, wakati Ndugai na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wanaingia wabunge wa CCM walianza kuimba wimbo wa chama chao, hali ambayo ilizua minong’ono miongoni mwa wabunge wakiwamo wa CCM.
No comments