Shughuli atakazofanya Makamu wa Rais Uganda,hizi hapa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameshawasili nchini Uganda na alipokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Philemon Mateke pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uganda Dkt. Aziz P. Mlima katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Entebe.
Makamu wa Rais pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaru wamesafiri na ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Tanzania aina ya Airbus A220-300 (Dodoma) kutoka jijini Dar es Salaam mpaka Entebe kupitia Kilimanjaro.
Kesho Makamu wa Rais atashiriki mkutano wa mwaka 2019 wa “Africa Now Summit 2019” ambao utafunguliwa na Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ambapo viongozi mbalimbali wa Afrika wanakutana ili kupata majibu ya changamoto za Afrika katika masuala ya kiuchumi.
Katika mkutano huo wa Viongozi wa Afrika, Makamu wa Rais anamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambapo katika mada mbalimbali zitakazojadiliwa Makamu wa Rais atazungumzia suala la Uongozi unaohitajika kuchochea mabadiliko ya Kijamii na Uchumi Afrika.
Viongozi wengine watakaotoa mada ni Rais wa Misri ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (UA) Mhe. Abdel Fattah el Sisi; Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa; Makamu wa Rais wa Kenya Mhe. William Ruto; na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Ahmed Abiy na Rais Paul Kagame wa Rwanda. Mada zote hizi zitajikita kwenye kuonesha chachu ya Uongozi katika kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.
Mkutano utamalizika tarehe 13 Machi 2019 utaanza na hotuba kutoka kwa Rais wa Somalia Mhe. Mohamed Abdullahi na baadae kufungwa rasmi na mwenyeji wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni.
Makamu wa Rais ataambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro.
No comments