Breaking News

Hotuba ya ACT Wazalendo kwa Viongozi wa Wilaya, Mkoa wa Kusini Pemba


Ndugu zangu mliokuwa  viongozi wa matawi, kata, majimbo na wilaya wa wilaya ya Mkoani, ninapenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wananchi wa Pemba kwa kumuunga mkono Maalim Seif katika uamuzi alioufanya yeye na wenzake kujiunga na chama cha ACT Wazalendo.

Pemba ilikuwa ngome ya CUF chini ya uongozi wa Maalim Seif. Kwa hivyo, kitendo cha mliokuwa wanachama wa CUF nyote kwa umoja wenu kujiunga na jukwaa jipya la siasa la ACT Wazalendo kinaifanya Pemba sasa kuwa ngome ya ACT. Hili ni jambo kubwa sana kwa chama chetu. 

Tumewapokea kwa moyo mkunjufu na mjihisi mmefika na mko nyumbani ndani ya ACT. Karibuni sana! 

Kisiwa cha Pemba na wananchi wa Pemba mna historia kubwa sana katika mapambano ya kupigania haki, demokrasia na utu. Pemba imekuwa ALAMA ya mapambano ya kupigania haki na demokrasia kabla na baada ya mfumo wa vyama vingi. 

Pemba mmekuwa Walimu na mmetufundisha Watanzania maana ya kuwa na Msimamo. Mmetufundisha maana ya ukweli katika kusimamia jambo mnaloliamini. Mmetufundisha maana ya kuwa utiifu kwa kiongozi mnayeamini anawakilisha na kusimamia kile mnachokiamini nyinyi. 

Kwa sababu ya Msimamo wenu, ukweli wenu na utiifu wenu kwa mnaloliamini na kulipigania, mmepitia katika hilaki na mateso makubwa sana. Pengine katika Tanzania hakuna eneo ambalo limeshuhudia hayo zaidi ya Pemba. Tunakuhakikishieni kuwa kujitoa kwenu si kwa bure na siku haiko mbali kile mlichokipigania mtakipata Inshallah kupitia jukwaa hili la ACT. 

Kuhusu suala la nafasi ya Zanzibar kwenye muungano, ninapenda kuwahakikishia kuwa Chama chetu kinaamini kuwa ili muungano wetu uwe wenye tija ni lazima kuwe na usawa baina ya pande zote mbili za muungano. Ndio maana katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2015, tuliweka bayana kuwa Chama chetu kinaamini katika Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ambayo ilishakamilisha wajibu wake wa kukusanya maoni ya wananchi kabla CCM na serikali yake haijayavuruga. Hivyo basi ninapenda kuwahakikishia Wazanzibar kuwa chama hiki kitakuwa jukwaa madhubuti la kuendeleza mapambano ya Wazanzibar katika kupigania muungano wa haki na usawa. 

Pemba ina matatizo mengi lakini kubwa ni ugumu wa maisha kutokana na kisiwa hichi kufungwa kisiweze kufurukuta. Vijana hawana ajira na mzunguko wa pesa ni mdogo sana. Tumekuwa watu wa kungoja kusaidiana tu. Haya ni maumivu kwa jamii ya watu inayojitambua na kuwa na fakhari ya utu wao. Maisha kama haya yanatufanya tuwe dhalili na kuudhalilisha utu wetu. Pemba ni kisiwa chenye fursa nyingi na watu wabunifu tena wachapa kazi. Pemba inahitaji kufunguliwa kiuchumi kwa kuunganishwa na Unguja, Dar es Salaam, Tanga na Mombasa. Pemba inahitaji kuunganishwa na dunia kibiashara. Haya hayawezi kufanywa na CCM. Tunahitaji mabadiliko ili tupate Serikali inayothamini watu na kuziona fursa zilizopo Pemba na kuzifungua. 

Tumekuja kukitambulisha Chama na kukupeni kadi za uanachama. Tutakuja tena kwa kazi ya kisiasa. Huku hamhitaji maelekezo. Nyinyi ndiyo walimu. Tutakuja tu kupeana hamasa ili kuhakikisha lengo lenu wananchi wa Zanzibar linafanikishwa. 

No comments