Waziri Jafo akerwa na kasi ya ukusanyaji mapato Kigoma Ujiji
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji inakabiliwa ugoigoi katika ukusanyaji wa mapato hali inayochangia kuzorota kwa shughuli za maendeleo ilhali ina rasilimali za kutosha.
Jafo alisema hayo kwenye uzinduzi wa Mfumo wa Kisasa wa Ukusanyaji Mapato kupitia Taarifa ya Kijiografia (GIS) uliounganishwa na mfumo wa mapato wa LGRCIS chini ya Mradi wa TSCP ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.
Alisema ugonjwa unaoisumbua Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ni 'unyafunzi' wa ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyake mtambuka, kitendo kinachokwamisha kutatua kero na changamoto zilizo ndani ya uwezo wake kupitia mapato ya ndani.
Alisema atashangazwa na manispaa hiyo endapo itashindwa kuonyesha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa weledi bila ujanja ujanja unaofanywa na watu wachache wanaohujumu uchumi ambao wanaathiri maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
"Nina sababu kubwa ya kutaka mabadiliko chanya katika ukusanyaji wa mapato. Huu ni mkoa wa kwanza kwa mgeni rasmi kuzindua mradi wa kisasa wa kitakwimu, uendelezaji na mkakati wa ukuaji wa miji ambao utakusanya mapato kwa mfumo wa taarifa za kijiografia uliounganishwa na mfumo wa mapato wa LGRCIS ili kudhibiti ugoigoi wenye mianya ya upotevu wa fedha za umma," alisema.
GIS ni kielelezo cha kubaini taarifa za kila mkazi na shughuli anayoifanya na taarifa zitaunganishwa na mfumo wa ukusanyaji wa mapato ili kubaini taarifa za walipakodi, huku akiwapongeza wataalamu wa mfumo huo wa kitakwimu (fungamano).
"Sasa msiichezee mifumo takwimu hii kwa maslahi binafsi. Fanyeni kama mfumo unavyotaka na tuwe waadilifu katika matumizi ya mfumo wa GIS kwa tija hata mataifa na halmashauri ziige taratibu za kitakwimu.
“Ajenda kubwa ya Rais John Magufuli na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kukusanya mapato yatakayotatua kero na changamoto za wananchi. Wakurugenzi wajibikeni msione haya kuuliza jambo kwa maslahi ya umma," alisema.
Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Mhandisi Mussa Natty, alisema wakusanyaji wa mapato walio wengi ni wadanganyifu wa makusanyo ambayo hayana taarifa ya takwimu za walipa kodi.
No comments