Breaking News

Waganga wa kienyeji 65 wadakwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma mauaji ya watoto



Jeshi la Polisi linawashikilia Waganga wa  kinyeji 65 kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya watoto yaliyotokea katika mikoa ya Njombe na Simiyu mwezi uliopita. 

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, amesema wanawashikilia waganga wa kienyeni 45 katika Mkoa wa Simiyu na wengine 20 wa Mkoa wa Njombe ambao wamewatilia shaka katika operesheni inayoendelea ya kuwasaka wahalifu hao. 

IGP Sirro ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu upelelezi wa matukio ya mauji ya watoto yaliyotokea katika Mkoa wa Njombe na Simiyu. 

"Kuna waganga ambao si wahalifu, lakini kuna wale waganga ambao ni wahalifu hao tunadili nao moja kwa moja na tayari tumeshakamata waganga 45 mkoani Simiyu na waganga 20 mkoani Njombe," alisema. 

IGP Sirro alisema sababu za kuwapo kwa matukio ya mauaji ni ramli chonganishi, ugomvi wa familia na wivu wa Mapenzi. 

"Zipo sababu nyingi zinazofanya kuwapo kwa matukio haya, lakini kubwa ni ramli chonganishi kwa maana hiyo operesheni zinaendelea kwa kila mganga, lazima wapekuliwe wakaguliwe na wale watakao onekana ni wahalifu na wanachofanya ni uvunjifu wa sheria, sheria itachukua mkondo wake," alisema IGP Sirro. 

Alisema pia wamezielekeza Halmashauri zifanye usajili wa waganga wa kienyeji na Viongozi wa dini na siasa ili wasaidie kutoa elimu kuhusu matukio hayo. 

Mwezi Januari, mwaka huu, kuliripotiwa matukio ya utekaji na mauaji dhidi ya watoto mkoani Njombe, huku wanaotekeleza ukatili huo wakidaiwa kunyofoa baadhi ya viungo kwenye miili ya watoto wanaowaua. 

Tayari watu kadhaa wamefikishwa mahakamani na kushtakiwa huku wengine wakiendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na matukio hayo. 

No comments