TCRA YATOA UFAFANUZI KUHUSU KUPUNGUZA GHARAMA ZA KUSAJILI MITANDAO YA KIJAMII 'BLOGS & ONLINE TV"
Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesema haiwezi kuzungumzia chochote kuhusu gharama za usajili wa mitandao ya kijamii inayotoa maudhui mtandaoni kwa sababu ni sheria na ili kupunguza gharama hizo lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa kupitia bungeni.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo wakati wa mkutano wa wadau wa sekta ya utangazaji kupitia Televisheni na Redio za kawaida na mitandaoni (Blogs & Online Tv) kutoka Kanda ya Ziwa Victoria uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Mhandisi Mihayo alitoa kauli hiyo akijibu swali la Mmiliki wa Malunde Media (Malunde 1 blog),Kadama Malunde aliyeiomba TCRA kupunguza gharama za usajili wa Mitandao ya Kijamii ili kuwasaidia vijana walioamua kujiajiri kupitia mitandao waendelee kutoa huduma za maudhui mtandaoni.
"Hizi gharama wanazotozwa hawa watoa huduma za maudhui mtandaoni ni ndogo ukilinganisha na zile gharama zinazolipwa na watu wa Televisheni na Radio, kwanza watu wa Mtandaoni wana leseni ya kimataifa, anapochukua habari anaenda kuzipakia kwenye mtandao zinaonekana dunia nzima lakini nyinyi (Tv na Radio) mna leseni kulingana na eneo husika",alisema Mhandisi Mihayo.
"Kwa hiyo Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) hatuwezi kuzizungumzia chochote hizi gharama za usajili kwa sababu ni sheria,sisi tunatekeleza sheria,kwa hiyo hizi gharama nafikiri ukitaka zipungue ni lazima mchakato wa kisheria ufuatwe kwa sababu lazima upitie bungeni",alieleza Mihayo.
Awali akitoa taarifa ya vituo vya utangazaji wa maudhui Kanda ya Ziwa, Mhandisi Mihayo alisema mpaka sasa Mitandao ya Kijamii iliyosajiliwa ni minne pekee ambayo ni Mohab Online Tv, Geita Online, Binagi Blog na Malunde Media huku akibainisha kuwa TCRA imewapa onyo na kuwataka watoa maudhui mitandaoni 24 kusajili Mitandao hiyo vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
" TCRA inawafahamu watu wote wanaopakia maudhui mtandaoni hivyo wale wanaoendelea kutoa maudhui mtandaoni ni lazima wafuate taratibu za kisheria ikiwemo kujisajili,tunaendelea kuwafuatilia na watashughulikiwa na vyombo vya kisheria",aliongeza.
"Kuna wale ambao wameamua kuhamishia kazi za blogs Instagram na Facebook, hawa nao tutawashughulikia",alisema Mhandisi Mihayo.
No comments